Breaking News

Uchumi katika Uislamu

Uchumi katika Uislamu

UTARATIBU wa maisha wa Kiislamu unamwongoza mtu kujenga na kudumisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, uhusiano wake na vinavyomzunguka katika ulimwengu huu na uhusiano wake na wanadamu wenzake. Pia unaratibu na kutoa mwongozo katika kila eneo la maisha ya mwanadamu. Eneo mojawapo la maisha ya mwanadamu ni uchumi. Yaani uzalishaji, usambazaji na utumiaji wa mali na huduma.
Uislamu umelipa suala la uchumi nafasi muhimu, umeweka taratibu zinazohakikisha kuwa haki inatendeka kwa wote ili kuleta amani, utulivu na mshikamano wa kweli katika jamii. Katika kuuangalia uchumi wa Uislamu tutajihusisha na maeneo yafuatayo:
1. Nadharia ya uchumi wa Kiislamu
2. Umuhimu wa uchumi katika Uislamu
3. Kanuni za uchumi katika Uislamu
4. Sera ya uchumi wa Kiislamu
5. Uhuru wa kuchuma
6. Mgawanyo wa mali
7. Mfumo wa benki katika Jamii
8. Tatizo la Riba
9. Haki ya kuhalalisha na kuharamisha
1. Nadharia ya uchumi wa Kiislamu
Mfumo wa uchumi wa Kiislamu si fani inayochunguza mwenendo wa mambo ya kiuchumi na kujaribu kuona kanuni zinazoratibu uchumi japo kuna kukaribiana kwa kiasi fulani mawili hayo. Mfumo wa uchumi katika Uislamu ni utaratibu utokanao na Qur'an na sunnah juu ya uzalishaji, umilikaji, usambazaji, na utumiaji wa mali na huduma pamoja na miiko yake. Kwa msingi huo, uchumi huo umejengwa juu ya fikra ya ukati na kati (Iqtisaad), hivyo umetofautiana na mifumo mingine iliyobuniwa na watu.
Dhana (concept) ya Iqtisaad katika shughuli za kiuchumi ni kule kutoa uhuru kwa mtu binafsi (sekta binafsi) kuchuma na kumiliki mali ili iwe motisha kwake ya kuchapa kazi wakati huo huo serikali kusimamia, na kutoa miongozo katika uendeshaji na ugawaji, na vile vile serikali kuwa na sekta zake ili kila mwana jamii atoe mchango wake wa nguvu, ufundi na utaalamu na apate haki na mahitaji ya kimsingi. Mifumo iliyobuniwa na watu imeathiriwa na udhaifu wa kibinadamu wa kuelemea upande huu au ule.
Ipo mifumo ya kiuchumi kama vile ya uchumi huria (Anarchism), umwinyi, ukabaila, ubepari, usoshalisti, ukomunist na ufashisti. Ubepari kwa mfano umeelemea mno katika ubinafsi kiasi ambacho umepuuza kabisa haki za kijamii. Katika mfumo huu (ubepari) umma hauna chake; mali, huduma na shughuli mbalimbali hubinafsishwa. Wachache chini ya mfumo huu ndio hunufaika na rasilimali za Taifa. Hujilimbikizia mali, na motisha yao ya uzalishaji ni ile faida waipatayo. Serikali kuu chini ya mfumo huu wa kibepari hushirikiana na wachache hao waliohodhi mali, kunyonya walio wengi(Islamic Economics: Theory and practice(A comperative study) by M.A.Manna.
Pia, kuna mfumo wa uchumi wa Kikomunist au Kijamaa ambao nadharia yake imeelemea mno katika "usawa" wa sare kiasi cha kudhoofisha mno motisha ya watu binafsi na hivyo kupelekea kukosekana kwa ufanisi katika uzalishaji. Katika mfumo huu mali na shughuli mbalimbali hutaifishwa (toka milki ya watu binafsi kuwa milki ya taifa) . Ukweli ni kwamba huwa si mali ya taifa kama inavyotangazwa bali mbiu ya "usawa" na "mali ya uma", chini ya mfumo huu, ni mwavuli tu unaokinga kikundi cha watu(system) kilichojipa mamlaka ya uendeshaji wa nchi kwa sura ya chama au serikali ambapo wachache hunufaika zaidi na rasilimali za nchi. Humiliki na kutafuna mali kwa hila mbalimbali huku wananchi walio wengi (proletariat majority) wakiendelea kuvuja jasho la damu viwandani, maofisini, mashambani na kwenye makampuni na mashirika ya "umma", kwa ujira hafifu usioweza kukidhi mahitaji ya lazima. Hivyo hakuna usawa wowote ulio chini ya mfumo huu bali ni ule ule ubinafsi wa kuhodhi mali na madaraka ambao hubadilika toka kuwa wa watu binafsi kwenda kwa kikundi (system)fulani.
Tofauti kati ya mfumo wa uchumi wa Kiislamu na ile ya Kijahili
Zipo tofauti kuu tano kati ya mwelekeo wa kiuchumi wa Kiislamu na ile ya Kijahili. Tofauti hizi ni:
(1) Dhana ya mafanikio:
Katika mtazamo wa uchumi wa Uislamu mafanikio yanatazamwa kwa kuzingatia hatima ya ama mtu kupata radhi za Mwenyezi Mungu au kubeba laana ya Mwenyezi Mungu. Mafanikio hayapimwi kwa wingi wa mali. Katika uchumi wa Kijahili mafanikio maana yake ni mafanikio ya kiuchumi. Ni kiasi gani cha mali mtu amefanikiwa kukipata. Jinsi atakavyojilimbikizia mali ndivyo itakavyoonyesha "mafanikio" yake. Katika Uislamu kufuzu kwa kweli ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kufeli kukubwa ni kule kukosa radhi hizo. Hivyo ili binadamu afanikiwe hana budi kuishi kwa uadilifu. Mtazamo huu unaathiri pia mizani yake ya wakati.Muislamu anapozitumia rasilimali zilizomo katika ardhi hafikirii tu mahitaji yake ya binafsi ya sasa bali pia matokeo ya vitendo vyake kwa vizazi vijavyo. Kwa mtazamo huu mtu anakuwa hana haki ya kufuja mali au rasilimali za ardhi, kwa vile anazingatia maslahi yake katika maisha haya, huko akhera na maslaha ya vizazi vijavyo.
Vile vile mafanikio katika Uislamu ni kule kulijua lengo la maisha hapa ulimwenguni, kuwa na kumbukizi ya kisimamo mbele ya Mola siku ya hesabu, kukinai moyoni na kukiona kila kitu cha ulimwengu huu kuwa ni cha kawaida. Kujitahidi kuyaendea mambo mema bila ya kuchelea chochote na kujiepusha na yale yote yanayoweza kukhasirisha katika maisha yajayo hata kama yana "manufaa" kwa mtazamo wa wengi katika maisha haya. Kujali shida na matatizo ya wengine na kuweza kutoa kuwasaidia wenye dhiki kwa kadiri ya wasaa. Kuwa na huruma, mapenzi na bashasha isiyobagua taifa, kabila, nasabu wala ukoo wa mtu. Kutokuwa na chuki, majivuno, kibri, utesi, usengenyi, ulimbukeni, kujiona, kujitukuza au kujidhalilisha na kujitweza kwa yeyote yule iwe kihali au kimali.
Aliyefanikiwa katika Uislamu ni yule ambaye neema yoyote aliyonayo haiwi kero na huzuni kwa wengine bali huitumia mwisho wa uwezo wake kuondoa Dhulma inayostawishwa na taratibu kinyume na Uislamu.
(2) Dhana ya mali:
Katika Uislamu mmiliki wa hakika wa mali ni Mwenyezi Mungu, mwanadamu kama Khalifa wa Allah hapa duniani anamiliki mali kwa dhamana tu siyo kwa hakika na kwa sababu hiyo ataulizwa jinsi alivyotumia hiyo mali. Pamoja na hivyo mali katika Uislamu si kitu kiovu bali kinachosisitizwa ni kuwa ichumwe na kutumiwa kwa kuzingatia maelekezo ya Mwenyezi Mungu. Kuhusu kutafuta mali Qur'an inatueleza kama ifuatavyo:
"Na utafute - kwa yale aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi mazuri ya akhera wala usisahau sehemu yako ya dunia" (28:77).
(3) Dhana ya bidhaa:
Katika uchumi wa kijahili kitu chochote chaweza kuwa ni bidhaa maadam kinaweza kutumiwa na mtu au mahali fulani. Kwa mfano pombe pamoja na madhara yake huitwa bidhaa kwa kuwa hutumiwa na baadhi ya watu.
Katika uchumi wa Kiislamu "bidhaa" huitwa ama "Atwayyibaati" au "Rizk". Atwayyibaat ni kitu kizuri, safi, Twahara . Rizk ni neema, au hidaya itokayo kwa Allah. Hivyo katika uchumi wa Kiislamu bidhaa ni vile vitu halali tu kwa mujibu wa sheria ya Kiislam. Kisichokuwa halali si bidhaa. Kwa mfano Pombe ni haramu hivyo si bidhaa.
(4) Dhana ya uadilifu katika utumiaji:
Kwa kuwa Allah ndiye muumba wa watu na rasilimali zote katika ulimwengu, sera ya uchumi ya Kiislamu haimpi mtu fursa ya kufuja mali apendavyo pamoja na uhalali atakaokuwa nao katika dhamana ya milki ya mali hiyo. Kinyume chake, katika uchumi wa Kijahili mtu anayo fursa kufuja mali apendavyo maadam ni mmiliki wa mali hiyo.
(5) Mizani ya wakati katika utumiaji:
Mtu anapofanya maamuzi yoyote hujiuliza nini matokeo au matazamio ya kitendo hiki au uamuzi huu baada ya saa moja au wiki moja au mwezi mmoja au mwaka mmoja au miaka mitano au kumi n.k. Kipimo cha wakati katika uchumi wa Kijahili na ule wa Kiislam ni tofauti. Katika ujahili mtu hujiuliza mali kiasi gani awe amepata atakapofikia umri fulani, kinyume chake Muislam anapofikiria jambo lolote, pamoja na masuala ya uchumi, kipimo chake cha wakati hukipa upeo mpana sana. Hujiuliza je, hiki kitendo ninachofanya kitakuwa na matokeo gani siyo tu kwa wiki hii au mwezi huu au mwaka huu au ujao bali kina matokeo gani siku ya kiyama.Muislamu anaamini kuwa ipo siku ya malipo na kwamba kuna pepo na moto.Watu watahesabiwa na kulipwa kwa mujibu wa matendo yao. Kila mtu binafsi atasimamishwa peke yake mbele ya Mwenyezi Mungu na kutoa hisabu yake. Imani hii ina athari kubwa kwa Muislamu na maamuzi yake anayochukuwa.


Hakuna maoni